Jumatano, 23 Novemba 2016

Msanii JUSTIN BIEBER Ampiga Ngumi Shabiki wake

Mwanamuziki asiyeishiwa matukio, Justin Bieber amezua sintofahamu baada ya kumchapa konde na kumpasua mdomo shabiki wake aliyekuwa akimlaki wakati akiwasili katika tamasha lake jijini Barcelona jana usiku.

Katika video fupi ya tukio hilo, staa huyo wa Pop mwenye miaka 22 kutoka nchini Canada anaonekana akimchapa konde shabiki huyo kupitia dirisha la gari alilokuwemo wakati akiwasili kwenye tamasha lake lililofanyika katika Uwanja wa Palau Sant Jordi uliopo jijini Barcelona.

Shabiki aliyepewa kichapo anaonekana akitaka kumshika staa huyo kupitia dirisha la gari kisha staa huyo anamtupia konde lililompasua mdomo.

Mara baada ya gari kuondoka, shabiki huyo anaonekana akishika mdomo wake uliokuwa ukivuja damu na baadaye kuanza kulalamika mbele ya kamera za wanahabari huku akizongwa na baadhi ya wanadada.

Imeelezwa kuwa shabiki huyo hakuripoti tukio hilo kwenye vyombo vya usalama ili Bieber achukuliwe hatua.

Source: GLOBALPUBLISHERS

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni