Alhamisi, 14 Aprili 2016

OmbaOmba Waanza kusombwa jijini DSM

POSTED THURSDAY, APRIL 14, 2016 | BY- VICKY KIMARO, MWANANCHI VKIMARO@MWANANCHI.CO.TZ

Ombaomba waanza kusombwa

Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limeanza kufanyiwa kazi baada ya karandinga

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limeanza kufanyiwa kazi baada ya karandinga kuanza kuwasomba ombaomba waliojaa katika maeneo mengi jijini hapa.

Makonda alitangaza kuanza kuwaondoa ombaomba hao juzi, huku akipiga marufuku wananchi kuwapa pesa kwa kuwa ndicho chanzo cha kuwapo kwao jijini hapa.

‘Mchakamchaka’ wa kuwaondoa watu hao ulianza juzi usiku katika maeneo ya Mnazi Mmoja, Samora na Kariakoo.

Mwananchi ilizunguka maeneo mbalimbali ambayo aghalabu ombaomba hupenda kukaa, lakini yalikuwa tupu.

Maeneo hayo ikiwamo barabara ya Morocco, Magomeni Usalama, Fire na Baridi hayakuwa na watu wa kundi hilo.

Mmoja wa ombaomba aliyekuwa na watoto wawili alipomuona mwandishi wa habari hizi katika maeneo ya Fire, alitimua mbio na kujificha pembeni mwa barabara, huku akisema: “Tumetoka Dodoma, hatutaki kurudi.”

Akizungumza na gazeti hili, Makonda alisema ikifika Jumatatu kama hawajajisalimisha Serikali itachukua hatua kali na kuwarudishwa walikotoka. “Kwanza ni kinyume cha sheria, pili ni hatari kwa maisha yao na watoto wanatakiwa warudi shule sasa,” alisema.

Kadhalika, operesheni hiyo licha ya timuatimua kuwakumba ombaomba, wapigadebe nao wameunganishwa katika kundi hilo kwa kuanza kuondolewa kwenye vituo vya mabasi.

Baadhi ya wapigadebe hao wamedai ni vigumu kwa Makonda kuwaondoa kwa kuwa wanachofanya ni kwa manufaa ya maisha yao na hawana pa kwenda.

Agizo la kutaka ombaomba wakamatwe na kuondokana na vitendo hivyo liliwahi kutolewa pia na waliowahi kuwa wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, Abbas Kandoro na Said Mecky Sadiki

Maoni 1 :

  1. Ni hatua nzuri sana ila je serikali imejipanga kukabili wimbi lao endapo watarudi kwa mfumo mwengne? Mm hapa naona hili si swala la kufumbia macho,kwa maana mambo kama haya yanaweza kupunguziwa utatuzi kwa kutumia sehemu ya mifuko ya jamii kuwainua walau wimbi la watoto wadogo wasio na hatia

    JibuFuta