Jumapili, 17 Aprili 2016

Ronaldo 'HATTRICK MACHINE' Mvunja rekodi Ulaya

Christiano Ronaldo

ADVERTISEMENT

CHEZA na wachezaji wote, lakini usimchezee Cristiano Ronaldo linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa. Anatisha kama njaa. Usibishe sana, rekodi zake zipo wazi na hat-trick ya juzi dhidi ya Wolfsburg ilikuwa ya tatu ndani ya msimu mmoja.

Hakuna mchezaji yeyote ambaye amewahi kufanya hivyo tangu kuanzishwa kwa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Lakini Ronaldo ana rekodi nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo itakusisimua na kumpigia saluti.

Ronaldo ni mchezaji pekee katika historia ya michuano hiyo kufunga mabao 15 na zaidi kwa misimu miwili mfululizo ikiwa ni baada ya kufunga mabao 17 msimu uliopita huku mabao yake matatu ya juzi yakimfanya afikishe idadi ya mabao 16 na anakaribia kuvunja rekodi yake mwenyewe.

Mashabiki wa Arsenal hawatapenda kuisikia hii. Ronaldo amefunga mabao matatu zaidi kuliko mabao yote ambayo Arsenal wamefunga katika Ligi ya mabingwa msimu huu. Mpaka sasa Arsenal wamefunga mabao 13 na wameshatolewa katika michuano.

Chelsea nao hawatapenda kuisikia hii. Mpaka sasa Ronaldo amefunga bao moja zaidi kuliko mabao yote ambayo Chelsea wamefunga katika Ligi ya Mabingwa msimu huu. wakati Ronaldo akiwa amefunga mabao 16, Chelsea imefunga mabao 15.

Kama vile haitoshi, Ronaldo ana rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko idadi ya mechi katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Amefunga mabao 40 katika idadi ya mechi 35 za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizochezwa dimba la Santiago Bernabeu.

Hakuna mechi muhimu zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kama mechi za mtoano. Ronaldo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 31, amefunga mabao 34 katika mechi 36 za mtoano za Madrid Ligi ya mabingwa Ulaya.

Kwa msimu huu, Ronaldo amezidi kuonyesha ubabe kwa wachezaji wenzake Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sababu amefunga mabao manane zaidi dhidi ya mastaa wawili wanaomfukuzia ambao ni Luis Suarez na Roberto Lewandowski wenye mabao manane kila mmoja.

Kama vile haitoshi, wote wanaosema Ronaldo huwa hajitokezi katika mechi muhimu wanakosea sana. Ronaldo amefunga mabao 15 katika mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ukijumlisha na mabao matatu aliyofunga juzi.

Ronaldo anaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa akiwa amefunga mabao 93 katika mechi 125 na hat trick yake ya juzi ilikuwa ya 37 tangu ahamie Madrid akitokea Manchester United kwa ada ya uhamisho wa dunia wa Pauni 80 milioni katika dirisha la majira ya joto mwaka 2009.

Kutokana na mabao yake ya juzi, Ronaldo ambaye msimu huu amejikuta katika wakati mgumu mbele ya mashabiki wake wa Santiago Bernabeu alijigamba kwamba mabao yapo katika damu yake na ataendelea sana kufunga.

“Haikuwa bora, lakini ulikuwa moja kati ya usiku wangu bora katika Ligi ya Mabingwa. Mabao yapo katika DNA yangu na nataka kuendelea kufunga kwa sababu ya timu,” alisema Ronaldo ambaye pia alizungumzia kuhusu rekodi yake ya upachikaji mabao.

“Ni wazi kwamba (Kufikia rekodi yake ya msimu uliopita) siyo kitu ninachokitafuta, lakini nina matumaini ya kuvunja rekodi hiyo na kufunga zaidi ya mabao 17. Itakuwa kitu kizuri. Itakuwa vizuri kwangu na kwa timu. Nitarajibu kadri niwezavyo,” alisema Ronaldo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni