Issa Mnally na Richard Bukos, UWAZI
Dar es Salaam: Mapya yameibuka kumhusu askari wa usalama barabarani (trafiki), Koplo Deogratius Mbango wa Kituo cha Oysterbay ambaye wiki chache zilizopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliagiza apandishwe cheo kutokana na kufurahishwa na utendaji kazi wake ambapo habari mpya ni kwamba, hadi juzi (Jumapili), bado hakuwa amepandishwa cheo kama rais alivyoagiza.
Trafiki huyo, alipata umaarufu mkubwa baada ya kumdhibiti dereva wa mke wa waziri mmoja (jina kapuni) aliyevunja sheria za usalama barabarani kwa kusimama kwenye alama za pundamilia (zebra) ambazo kimsingi hutumiwa na watembea kwa miguu wanaovuka barabara.
Akiwa anatekeleza majukumu yake, Aprili 24, mwaka huu, inadaiwa kuwa mke wa waziri aliyekuwa amebebwa ndani ya gari hilo, amlijia juu Koplo Deogratius huku akimtolea vitisho kwa kutumia cheo cha mumewe, lakini askari huyo hakutetereka zaidi ya kuendelea kusimamia sheria na kuwataarifu wakubwa wake wa kazi, akiwemo Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kinondoni (RTO) Awadh Haji.
Katika uchunguzi wake wa chini kwa chini, Uwazi limebaini kuwa bado askari huyo anaendelea kukitumikia cheo chake cha zamani, jambo ambalo ni kinyume na maagizo aliyoyatoa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Magufuli.
Ili kujiridhisha zaidi, Uwazi liliwahoji baadhi ya watu wa karibu wa askari huyo ambao kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini kwani siyo wasemaji, walisema Koplo Deogratius hajapandishwa cheo kama Rais Magufuli alivyoagiza kwani kama ingekuwa hivyo, angekuwa anaonekana.
Uwazi halikuishia hapo, lilimtafuta Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga na kumuulizia sababu zilizokwamisha afande huyo kupandishwa cheo mpaka sasa ambapo alisema:
“Aaah ni kweli ndugu mwandishi hilo agizo lilitolewa na rais lakini hata mimi sijui kwa nini hajapandiswa cheo mpaka leo. Unajua suala la upandishwaji wa vyeo vya kipolisi hata hawa wa usalama barabarani walio chini yangu, huwa sihusiki bali anayewapandisha ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu. Muulize mwenyewe au mtafute msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimbo wao ndiyo watakaoweza kukupa majibu ya uhakika.”
Gazeti lilianza kumtafuta Advera kwa njia ya simu ambapo simu yake haikuwa hewani kila alipopigiwa. Baada ya kumkosa, Uwazi lilimtafuta, IGP Mangu kwa njia ya simu lakini naye simu yake haikuwa hewani kila alipopigiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni