Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.
Nicodemus Jonas,Dar es Salaam
KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni zaidi ya upinzani wa jadi, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ametangaza kumfikisha Polisi Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro kwa kile alichobainisha kuchoshwa kudhalilishwa, kushutumiwa na kutukanwa.
Manara ametoa kauli hiyo jana huku akidai Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa kimya na halimchukulii hatua Muro, pamoja na kuwa kimya kutotolea majibu madai kadhaa ya Simba hasa yanayohusu Yanga.
Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro.
“Simba tumechoshwa na kauli za Muro na iwapo kamati ya maadili ya TFF itashindwa kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kauli zake, basi ishu itafika polisi kwani kuna kesi ya jinai,” alisema Manara na kuendelea:
“TFF imekuwa kimya kwa mambo mengi likiwemo lile la Donald Ngoma (Yanga) kumpiga kichwa Hassan Kessy (Simba) katika mchezo wa raundi ya kwanza.
“TFF bila hata Simba kusema lolote, wao wenyewe walitangaza kumchukulia hatua za kinidhamu Muro kwa lugha ya kibaguzi, kudhalilishana lakini hakuna kilichofanyika.
“Muro amekuwa na rekodi ya kesi pale TFF, amewahi kumdhalilisha kiongozi wa Bodi ya Ligi akawatukana Kimondo FC, kesi yangu ipo pale, kwa nini jamani?
“Tutakwenda polisi, tulitaka haya mambo yaishe kimichezo lakini kama hawatachukua hatua, litafika polisi.”
Akijibu madai hayo, Muro alisema: “Ni bora aende huko kuliko kupiga ‘porojo’. Kwani ni uongo kusema kocha wao amekuja kwa basi na wetu amekuja kwa ndege? Si wamemsajili kutoka Coastal pale Tanga na wetu ni Mholanzi amekuja kwa ndege! Kama anaamini amedhalilishwa aende kwenye vyombo vya dola akashtaki.”
Kutokana na kuingia katika migogoro mara kadhaa, wahusika hao wamebandikwa majina ya Tom na Jerry na baadhi ya watu mitaani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni