Jumatatu, 1 Februari 2016

Tambwe:Kiiza haniwezi


ADVERTISEMENT


HEBU piga picha. Upande huu wa Msimbazi kuna Hamis Kiiza, kule Jangwani kuna Amissi Tambwe ambao kazi yao ni kutupia tu mabao. Kwa ukali wao huo wa kufumania nyavu kweli kuna timu itakayopona?
Kiiza amefikisha mabao 12 mpaka sasa, baada ya juzi Jumamosi kufunga mabao mawili wakati Simba ikiizamisha African Sports kwa mabao 4-0, hivyo kubakisha bao moja tu kumfikia Tambwe mwenye mabao 13 akiongoza orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara msimu huu.   
Licha ya kasi ya Mganda wa Simba, Tambwe amemwambia Kiiza kwamba kamwe hawezi kumpata kwenye uwaniaji wa Kiatu cha Dhahabu.
Straika huyo wa Yanga anayetokea Burundi aliliambia Mwanaspoti kuwa anafahamu Kiiza ni mzuri na anamfukuzia kwenye upachikaji wa mabao lakini mbio zake haziwezi kumpita kwani anaamini yeye ni mkali kuliko Kiiza.
“Kiiza hawezi kunipata, nitajitahidi kwa kila hali ili niwe mbele zaidi yake. Hii ligi ni ngumu na ina upinzani mkubwa, tumepoteza mechi moja tunatakiwa kushinda mechi zote zilizobaki,” alisema Tambwe ambaye juzi Jumamosi alishindwa kuisaidia timu yake isiaibike Mkwakwani Tanga.
Yanga ilipoteza mechi yao ya kwanza katika msimu huu baada ya kucharazwa mabao 2-0 na Coastal Union katika pambano hilo lililovutia wengi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni