Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI na mitandao
DAR ES SALAAM: Lile sakata wa mwanafunzi wa kike Mtanzania (jina linahifadhiwa), kupigwa, kuvuliwa nguo na kisha kulazimishwa kutembea akiwa uchi limetolewa undani wake, Uwazi lina mlolongo wote.
Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 anayesoma Shahada ya Biashara, mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Acharya, Bangalore nchini humo, alifanyiwa ukatili huo akiwa na Watanzania wengine wanne.
GAZETI LA INDIA LILIANZA KUFICHUA
Gazeti la Deccan Chronicle la Mji wa Bangalore ndilo lilikuwa la kwanza kuandika habari hiyo iliyojiri Januari 31, mwaka huu na hivyo kuufungua macho ulimwengu juu ya tukio hilo la kikatili.
BADO YUPO HOSPITALI
Baada ya mwanafunzi huyo kutendewa unyama huo, baadhi ya Watanzania wamesema alifariki dunia katika eneo la tukio lakini ukweli ni kwamba, majeruhi huyo bado amelazwa kwenye Hospitali ya Peenya iliyopo Bangalore nchini humo.
WATANZANIA WAUNGANISHA
Kumekuwa na picha kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ya mwanaume anayedaiwa kuwa ni Mtanzania ambaye alifariki dunia nchini humo kwa ajali ya pikipiki ambapo vyanzo vinasema alijipiga kwenye nguzo ya pembeni mwa barabara.Picha hiyo, ndiyo wengi wamekuwa wakiitumia kusema ni ya mwanafunzi Mtanzania aliyedhalilishwa.
MWANAFUNZI MBONGO
Akizungumza na Uwazi juzi, mwanafunzi mmoja anayesoma kwenye chuo hicho, alisema bado tukio hilo linawagonga vichwa wanafunzi wote Waafrika licha ya Serikali ya India kuchukua hatua inayostahili, ikiwemo kuwawekea ulinzi wanafunzi wa Kitanzania.
MWANAFUNZI ASHAURIWA KURUDI
“Watu wanaweza kusema mengi lakini ni tukio lenye kumbukumbu mbaya sana kwa mwenzetu. Ubaguzi ulitawala kwa wale wachache waliohusika. Tunafikiria kwamba, akipata nafuu arudi nyumbani kupumzika. Kwani kwa kuendelea kusoma sidhani kama ataingiza ‘matirio’ kichwani.
“Kwanza tukio limemjengea hofu. Halafu bado atakuwa katika mji huuhuu na watu atawaona walewale. Vyema arudi kupumzika. Lakini ni ushauri tu, si lazima iwe hivyo na pia itategemea ujasiri aliozaliwa nao,” alisema mwanafunzi huyo akiomba hifadhi ya jina lake.
ILIVYOKUWA
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, siku ya tukio, raia wa Sudan aitwaye Ismail Ahad Mohammed (20) inayedaiwa alikuwa ‘amekunywa’, alimgonga mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35, mkazi wa Mji wa Hesaraghatta na kusababisha kifo chake.
KILICHOTOKEA SASA
“Sasa baada ya dakika kama thelathini hivi kupita, Watanzania watano, akiwemo dada yetu aliyevuliwa nguo, walifika eneo hilohilo wakiwa ndani ya gari dogo. Ndipo kundi la watu walipoanza kuwashambulia akiwemo dada yetu. Washambuliaji waliona ni walewale tu.”
UKATILI ULIPO
“Kuwashambulia tumechukulia ni sehemu ya hasira za kuona watu ni walewale, lakini sasa kitendo walichomfanyia sista wetu cha kumvua nguo na kumlazimisha atembee uchi ndiyo kilikuwa kibaya sana.
“Lakini pia kundi hilo la watu lilichoma moto lile gari la kwanza lililosababisha ajali mpaka akafa mwanamke na pia walichoma moto gari alilokuwemo dada yetu na wenzake. Wengine walikimbia lakini dereva wa gari la pili naye alishambuliwa, gari la kwanza alikamatwa na polisi.”
LAWAMA ZA POLISI
Polisi wa mji huo wamebebeshwa lawama kwamba licha ya kuwepo eneo la tukio lakini hawakuchukua hatua yoyote. Mbaya zaidi, mwanaume mmoja raia wa nchi hiyo alijitolea kumsitiri mwanafunzi huyo kwa kumpa T-Shirt (fulana) yake lakini watu hao walimpiga na kuichanachana nguo hiyo.
UKATILI KWENYE DALADALA
Kuna maelezo kwamba, mwanafunzi huyo alipoona hali inazidi kuwa mbaya, alikimbilia kwenye ‘daladala’ la huko akiamini kwamba litaondoka hivyo yeye kunusurika na kipigo na kusitiriwa kwa nguo lakini baadhi ya abiria walimshusha ili aendelee kudhalilishwa hivyo kumfanya aendelee kuwepo mtaani akitembea bila nguo.
DEREVA APIGWA
Mshauri wa masuala ya sheria kwa wanafunzi kutoka Afrika wanaosoma Bangalore, Bosco Kaweesi alisema naye dereva wa gari alilokuwemo Mtanzania huyo, Micah Pundugu alipigwa na kujeruhiwa vibaya.
WATANZANIA BONGO WAONGEA
Baadhi ya Watanzania hapa Bongo wameongea na Uwazi na kuonesha mtazamo wao kuhusu sakata hilo.
Musa Ibrahim, mkazi wa Mabibo jijini Dar yeye alisema:
“Kwa kweli sisi hapa nyumbani Tanzania tunaishi kwa upendo mkubwa na hawa ndugu waishio hapa. Kwa hiyo walichofanya wale si haki. Lakini bahati nzuri ni kwamba, kitendo kile hakijaungwa mkono na raia wote wa nchi ile.
“Ndiyo maana kuna raia alijitolea fulana, lakini pia Serikali ya India imechukua hatua kali sana kwa wahusika ambao wamekamatwa, polisi wamesimamishwa kazi, wengine kufukuzwa.”
Mama Prince, mkazi wa Kimara Baruti yeye alisema: “Mimi sikubaliani kama tukio lile lilikuwa la kila raia wa kule. Ni wale wakorofi tu.
Mbona hata hapa nyumbani kuna Watanzania wanaweza kufanya vile kwa Watanzania wenzao. Unajua kila nchi ina watu wakorofi, wakatili na wapuuzi. Sasa upuuzi wa watu wachache usiwapake matope wote. Ila kama Serikali ya India ingekaa kimya, hapo sasa naamini moto wake ungekuwa mkubwa.”
BALOZI WA TANZANIA
Naye Balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi alisema ameridhika kwa namna ambayo serikali ya nchi hiyo imeweka mikakati ya kutosha kuwalinda wanafunzi kufuatia kisa hicho.
“Cha muhimu ni kuangalia siku za mbele kwa sababu tusipofanya hivyo tutapotea. Tunahitaji kutatua tatizo la sasa lakini pia tuangalie mikakati ya muda mrefu,” alisema Balozi Kijazi.Akaendelea: “Nimeridhishwa na hatua za kiusalama ambazo zimechukuliwa na Serikali ya India kwani kuna maafisa ambao wamesimamishwa kazi mara moja.”
KILICHOJIRI BAADA YA TUKIO
Mpaka sasa, watu tisa wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku
Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Soldevenahalli akisimamishwa kazi kwa tuhuma kwamba, hakuchunguza kwa undani kisa hicho baada ya mmoja wa wanafunzi hao kutoa taarifa kituoni na konstebo wa polisi mmoja pia amesimamishwa kazi kwa kutochukua hatua kuzuia wanafunzi hao wasishambuliwe na umati.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augostine Mahiga wiki iliyopita Bungeni Dodoma alitolea ufafanuzi sakata hilo jinsi Serikali ya India inavyolishughulikia na kumfanya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kutokwa na machozi kwa uchungu wa simulizi yenyewe.
Gazeti hili bado linachimba habari hii baada ya kuwepo madai kwamba, mwanafunzi huyo atarejeshwa nchini wakati wowote huku akidaiwa kuwa ni mzaliwa wa Mkoa wa Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni