Jumatatu, 8 Februari 2016

Makamishna Wa Uchaguzi ZEC Wapinga Uchaguzi Kurudiwa

uchaguzi Z’bar

 0

 0

 0

 0

 0

 0

 0

 

Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Ayoub Bakari Hamad akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana kuhusu uchaguzi wa marudio visiwani humo. Kushoto ni mjumbe mwenzake, Nassor Khamis Mohammed. Picha na Salim Shao 

Kwa ufupi

Wajumbe hao wa chombo hicho cha uchaguzi pia wamesema hoja ya kupanga tarehe mpya ya uchaguzi iliyopendekezwa na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha ilipingwa na wajumbe watatu na kuungwa mkono na wengine watatu.

By Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Dar es Salaam. Makamishna wawili wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wamejitokeza hadharani na kutangaza kupinga kurudiwa kwa uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani, uamuzi wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 uliofanywa na mwenyekiti badala ya tume kinyume na sheria.

Wajumbe hao wa chombo hicho cha uchaguzi pia wamesema hoja ya kupanga tarehe mpya ya uchaguzi iliyopendekezwa na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha ilipingwa na wajumbe watatu na kuungwa mkono na wengine watatu.

Makamishna hao, Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Bakar Hamad walisema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kwamba uchaguzi uliofanyika Zanzibar hautafutika kwa kuwa ulikuwa halali kikatiba.

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, akisema kulikuwapo na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi na miezi miwili baadaye aliitangaza Machi 20 kuwa tarehe mpya ya kupiga kura.

Uchaguzi huo ulifutwa siku ambayo mshindi wa kiti cha urais alitakiwa atangazwe, huku matokeo ya majimbo 31 yakiwa yameshatangazwa na kura katika majimbo mengine tisa zikiwa zimeshahesabiwa. Pia, washindi wa nafasi za uwakilishi na udiwani walishatangazwa na kupewa hati za ushindi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Nassor aliwataka wajumbe wenzake wa ZEC kutounga mkono uchaguzi wa marudio ili wasiwe sehemu historia mbaya ya nchi hiyo.

Alisema kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar hakitoi nafasi kwa mwenyekiti peke yake kufanya uamuzi wa kufuta matokeo kwa jina la tume.

“Uamuzi mkubwa uliofanywa na mwenyekiti hauwezi kuchukuliwa kuwa uamuzi wa Tume na kurudia uchaguzi ni kuiweka nchi katika majaribu,” alisema.

Nassor alisema uchaguzi wa Zanzibar ulishakamilika katika ngazi za uwakilishi na udiwani huku wateule katika nafasi hizo wakikabidhiwa vyeti vyao kuthibitisha ushindi wao.

“Hakuna chombo chochote kinachoweza kubatilisha uchaguzi isipokuwa Mahakama Kuu baada ya kusikiliza shauri. Hao ndio ambao wametajwa kwenye sheria ya uchaguzi,” alisema.

Alisema uchaguzi wa rais wa Zanzibar haukulalamikiwa na mgombea yoyote kati ya 14 waliowania nafasi hiyo.

Nassor alisema yeye na wenzake wameendelea kuwepo kwenye tume hiyo ili kutoa ushauri kwa wenzao na pia kujua kinachoendelea na kuwafahamisha wananchi.

“Kwa hali ya Zanzibar ilivyo sasa anahitajika mpatanishi wa kimataifa ambaye ataziweka pande mbili za vyama vya siasa zinazotofautiana kisiasa katika meza ili kufikia suluhu,” alisema.

Kwa upande wake, Ayoub alisema Jecha anatakiwa kujipima, afanye uamuzi mgumu ili kuiepusha nchi kuingia katika vurugu.

Alisema kama uchaguzi huo ukifanyika, utatoa viongozi batili kwa sababu uchaguzi halali Zanzibar ulishafanyika.

Nassor alidai kuwa siku mbili baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar, Jecha aliitisha kikao na kuomba wajumbe waunge mkono uamuzi huo, lakini nusu ya wajumbe walimuunga mkono na wengine walipinga.

Alisema Januari 21, mwaka huu tume ilikuwa na kikao kingine ili kujadili tarehe ya uchaguzi wa marudio.

“Baadhi ya wajumbe waliamua kuwa Machi 20, 2016 iwe ndiyo siku ya uchaguzi na wengine walipinga uchaguzi wakisema ufutaji wa matokeo ulikuwa batili kikatiba na kisheria,” alisema.

Alisema wakati Rais John Magufuli anachukua hatua nzito kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, nchi yenye uchumi mdogo kama Zanzibar inatumia zaidi ya Sh7 bilioni kufanya uchaguzi wa marudio.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni