=
WEDNESDAY, FEBRUARY 3, 2016
Funga mkanda yawakuna wasomi
0
Kwa ufupi
Katika mwongozo huo, Dk Mpango aliainisha mambo kadhaa ambayo ni vipaumbele vya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17 na kutaja mbinu za ukusanyaji mapato, kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza mapato ya kodi na kupunguza matumizi ya Serikali.
By Florence Majani, Mwananchi fmajani@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mpango wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/ 2017 uliotolewa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango katika hotuba yake umepongezwa na wachumi huku wakiwa na wasiwasi kuhusu utekelezaji wake.
Katika mwongozo huo, Dk Mpango aliainisha mambo kadhaa ambayo ni vipaumbele vya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17 na kutaja mbinu za ukusanyaji mapato, kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza mapato ya kodi na kupunguza matumizi ya Serikali.
Mengine ni kuimarisha viashiria vya uchumi na maendeleo, marejesho ya kodi, kupunguza gharama, kukuza pato halisi la Taifa na kupunguza nakisi ya Serikali kwenye misaada ya nje kwa zaidi ya asilimia tatu.
Kuimarisha mapato ya ndani
Katika hotuba yake, Dk Mpango alisema shabaha ya bajeti ya mwaka 2016/17 inalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kufikia asilimia 14.8 ya Pato la Taifa. Alisema mapato hayo yanatakiwa yafikie asilimia 15.3 mwaka wa fedha 2017/18 na asilimia 16.3 ifikapo 2019/20.
Ukusanyaji wa mapato
Katika ukusanyaji wa mapato ya kodi ili yafikie asilimia 13.2 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 na asilimia 13.5 mwaka 2019/20, Dk Mpango alisema Serikali imefuta usimamiaji wa mapato unaofanywa na taasisi za Serikali na badala yake mapato hayo yatakusanywa na Wizara ya Fedha na Mipango.
Maeneo mengine ni kukusanya kodi za majengo, kurasimisha biashara ambazo hazijarasimishwa na kusimamia upatikanaji wa matumizi sahihi ya mashine ya EFD.
Kadhalika, hotuba hiyo ilisisitiza kupitiwa upya mikataba iliyopewa misamaha ya kodi.
Katika kipindi cha 2016/17 bajeti hiyo ililenga kukusanya jumla ya Sh14.1 bilioni kutoka kwenye vyanzo vya ndani ambayo ni asilimia 13.2 ya pato la ndani. Hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.
Pato la Taifa na mfumuko wa bei
Aliitaka shabaha kuu kuwa ni kukuza pato halisi la Taifa kutoka asilimia saba mwaka 2015 hadi asilimia 7.2 kwa 2016 na kufikia asilimia nane 2017.
Mwongozo huo ulilenga pia kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki kwenye tarakimu moja na kufikia asilimia sita Juni 2016 na kubaki kati ya asilimia tano na nane katika kipindi cha muda wa kati.
Kupunguza matumizi
Waziri alisema Serikali ina mpango wa kupunguza matumizi yake kutoka asilimia 23.9 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 hadi asilimia 21.5 mwaka 2016/17.
Pia alitaka mashirika ya umma; Tanesco, Tazara, Shirika la Reli (TRL) Shirika la Ndege (ATCL) na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), yajitegemee na kutengeneza faida badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali.
Bajeti ya Serikali
Dk Mpango alisema bajeti hiyo inatarajia kupunguza nakisi ya Bajeti ya Serikali kwenye misaada ya nje kutoka asilimia 4.2 mwaka 2015/16 hadi chini ya asilimia 3.0.
Jumla ya Sh22, 991. 5 bilioni zinatarajiwa kukusanywa. Kati ya hizo, mapato ya ndani na ya halmashauri yataongezeka na kufikia Sh15,801 bilioni sawa na asilimia 69.7 ikilinganishwa na asilimia 62.2 ya 2015/16.
Katika jumla hiyo, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa Sh584 bilioni, pia Serikali itakopa kiasi cha Sh1,782 bilioni kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara, mikopo ya ndani Sh3,300 bilioni na wadau wa kimaendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh2,107 bilioni katika kipindi hicho.
Changamoto za nusu ya 2015/16
Licha ya kutoa shabaha ya bajeti ya mwaka 2016/17, Dk Mpango alieleza changamoto zilizoonekana kwenye bajeti ya nusu mwaka ya 2015/16 kuwa ni ukwepaji kodi kwa wafanyabiashara wasio waadilifu, mwitikio hasi kwenye matumizi ya EFD, kuongezeka kwa matumizi ya Serikali kusikowiana na hali halisi ya mapato na mazingira magumu ya ukusanyaji wa kodi katika sekta zisizo rasmi.
Wachumi wazungumzia mwongozo
Akizungumzia mkakati wa Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alipongeza mpango huo akisema katika Awamu ya Nne, Serikali ilikithiri kwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha.
“Dk Mpango amefanya vyema kuweka hilo kwenye mwongozo. Kwa mfano, wabunge wasifanye sherehe zisizo za lazima na kupunguza safari za nje, yote hiyo ni azma ya kubana matumizi. Hilo tunalipongeza,” alisema.
Alisema hata Uchaguzi Mkuu ulikuwa na matumizi makubwa yasiyo ya lazima kwani hakukuwa na haja ya kununua magari ya polisi 770 wakati wa uchaguzi.
Kuhusu mashirika ya umma, Profesa Mpangala alisema yakifanya kazi kwa ufanisi yanaweza kujiendesha lakini kikwazo ni ufisadi na rushwa.
“Lakini suala si haya mashirika kujitegemea tu, bali kuweka mikakati dhabiti na kuondoa vikwazo vinavyofanya yasiendelee,” alisema.
Kuhusu mfumuko wa bei na ukusanyaji wa mapato, mchumi na mtafiti wa maendeleo wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema kwa kuwa uongozi wa sasa unaonekana makini, malengo hayo yatawezekana.
“Uongozi wa sasa si holela holela, watekelezaji wamefanya kazi yao. Kule kubana matumizi ni sawasawa ili fedha zihudumie watu na si watumishi,” alisema.
Mhadhiri wa uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Stephen Kirama alisema miongozo na shabaha iliyotolewa na Waziri wa Fedha ni ya kisomi lakini ina changamoto kadhaa. Alisema kumlazimisha mfanyabiashara kutumia mashine za EFD ni jambo la moja na kuzitumia ni jambo jingine. “Lakini je, watu watakubali kudai risiti?” alisema.
Aliongeza zaidi kuwa katika suala la ukusanyaji wa kodi atakutana na changamoto za kutambua, kuorodhesha, kurasimisha na namna gani watachukua mkakati wa kukusanya kodi.
Kuhusu kupunguza utegemezi wa fedha za wahisani katika bajeti hadi kufikia asilimia chini ya tatu, Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu, Godfrey Bonaventure alisema ili kufanikisha hilo ni lazima Serikali ipanue wigo wa ukusanyaji mapato.
Alisema ni lazima bajeti iendane na matumizi kwa kuhakikisha inakusanya mapato kutoka vyanzo vikuu vya mapato.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni