Ijumaa, 26 Februari 2016

Majambazi Wavamia Benki Mbagala

Majambazi Dar yavamia benki yapora yaua, yauawa

Majambazi ambao idadi yao haikufahamika wakiwa na mabomu na bunduki za kisasa jana walivamia

Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya tawi la Benki ya Access lililopo Mbagala, Dar es Salaam baada ya kuvamiwa na majambazi na kupora fedha. Picha na Raymond Kaminyoge

Dar es Salaam. Majambazi ambao idadi yao haikufahamika wakiwa na mabomu na bunduki za kisasa jana walivamia benki ya Access, tawi la Mbagala wakapora viroba vya fedha, wakaua mlinzi na baadaye wanne kati yao wakauawa na polisi

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema baada ya majambazi hao kufika katika benki hiyo kwa bodaboda nne majira ya saa nane mchana, yalimuua mlinzi wa benki hiyo, kisha kubomoa kwa risasi mlango wa vioo na kuingia ndani na kuzua taharuki kubwa.

Mashuhuda hao walisema katika tukio hilo lililodumu kwa karibu saa moja, mmoja wa majambazi hao aliyekuwa amevaa kininja, alikuwa barabarani akiamuru magari kupita haraka huku akifyatua risasi ovyo.

Ilielezwa kuwa jambazi huyo aliyeonekana kuwa na uzoefu na matumizi ya bunduki alikuwa akifyatua risasi kwa kutumia mkono mmoja na ndiye aliyewajeruhi  baadhi ya wapita njia.

Hivyo, wakati uporaji ukiendelea na jambazi huyo akiimarisha ulinzi barabarani baadaye hakukuwa na magari wala pikipiki zilizokuwa zikipita.

Mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi jirani na benki hiyo, Ramadhani Tairo alisema  baada ya  jambazi huyo kuliona gari la polisi likielekea eneo hilo, alifyatua risasi na kulipiga kabla halijafika ma kupoteza mwelekeo na kutumbukia kwenye mtaro.

Tairo alisema mbali ya jambazi hilo kulipiga risasi gari la polisi pia alilirushia bomu la mkono,  lakini liliangukia barabarani bila kulipuka. Polisi walifanikiwa kulitegua bomu hilo baadaye likiwa halijasababisha madhara kwa wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Rebeca Maliva alisema majambazi walioingia ndani ya benki hiyo walionekana wakitoka wakiwa na viroba vitatu vya fedha ambavyo walivipakata kwenye pikipiki na kuondoka kwa kasi kuelekea Mkuranga kupitia barabara ya Kilwa.

Rebeca alisema polisi zaidi walifika kwenye eneo hilo wengine wakiwa kwenye pikipiki na kuanza kuwafukuza majambazi hao ambao walipofika eneo la Shule ya St Mary’s, walitupa  kiroba kimoja ambacho wananchi waliokuwa jirani waligombania na kuchukua fedha zilizokuwamo.

“Baada ya milio ya risasi nilikuwa nimejifungia ndani nikawa nachungulia nje nikawaona watu wanagombea fedha, kila mtu aliyekuwa hapo alionekana na burungutu la noti na kukimbia,” alisema Rebeca ambaye yeye na familia yake hawakuthubutu kutoka.

Baada ya nusu saa wakati umati ukiwa bado kwenye benki hiyo, magari ya polisi yalipita katika eneo hilo yakitokea eneo la Mkuranga  yakiwa yamebeba miili ya majambazi waliouawa.

Magari hayo yalikuwa yakisindikizwa na vijana wa bodaboda waliokuwa wakishangilia kazi  iliyofanywa na polisi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alizungumzia kwa ufupi tukio hilo kwamba majambazi manne yaliuawa na kukamata silaha tatu, lakini hakutaka kuingia kwa undani akisema atatoa taarifa zaidi leo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni