Alhamisi, 21 Januari 2016

Air Tanzania yafufuka rasmi

Hatimaye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limefanikiwa kuifufua ndege yake aina ya De-Havilland

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila akishuka kwenye Ndege ya Air Tanzania katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Saalam leo

Dar es Salaam. Hatimaye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limefanikiwa kuifufua ndege yake aina ya De-Havilland Dash 8 Q300 baada ya kufanyiwa ukarabati kwenye karakana ya shirika hilo iliyopo jijini Dar es Salaam

Ndege hiyo ambayo imeanza safari zake rasmi leo asubuhi kutoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Kigoma na kurejea mchana, ina uwezo wa kubeba abiria 50.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) baada ya kuwasili kutoka mkoani Kigoma, Mhandisi wa shirika hilo, Righton Mwakipesile amesema kabla ya kuanza kufanya safari zake rasmi, ndege hiyo ilifanyiwa ukaguzi na wataalamu kutoka Mamlaka ya Usalama wa Anga nchini (TCAA) na kuiruhusu kuendelea na safari.

Amesema matengenezo ya ndege hiyo kwa kiasi kikubwa yamefanywa na mafundi wa kizalendo. “Baada ya ukaguzi kufanyika, TCAA ilitoa cheti cha kuthibitisha kuwa ndege hii ni salama kwa kuruka na kwamba, imekidhi viwango vya ubora,” alibainisha Mhandishi Mwakipesile.

Akizungumzia mafanikio hayo, Ofisa Uhusiano wa Shirika hilo, Lilian Fungamtama amesema ni sehemu ya mkakati wa shirika kuhakikisha kuwa linaboresha na kupanua huduma zake ili kuendana na mahitaji ya soko na hadhi yake nchini.

“Kurejea kwa huduma za ndege hii kutatuwezesha siyo tu kuwa na uhakika wa safari zetu kuelekea mkoani Kigoma, bali pia baada ya siku chache zijazo kuongeza safari moja kuelekea mkoani Mwanza na kufanya ziwe mbili kwa siku huku pia tukitarajia kurejesha safari zetu kuelekea mkoani Tabora, Kilimanjari na Zanzibar,’’ amesema Lilian.

Kwa upande wa baadhi ya abiria waliosafiri na ndege hiyo leo, wamesema wameridhishwa na huduma zitolewazo na ndege hiyo.

Abiria Moses Chuwa amesema kuanza kwa safari za ndege hiyo kuelekea Kigoma, kutawapunguzia adha ya kusafiri kwa muda mrefu kuelekea mkoani humo kwa basi.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni