Sheria ya Magazeti yalifuta Mawio
Gazeti la kila wiki la Mawio limekuwa la kwanza chini ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo (Usajili), Raphael Hokororo. Picha na Salim Shao
Dar es Salaam. Gazeti la kila wiki la Mawio limekuwa la kwanza chini ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano (SAT) kufungiwa, baada ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye kutangaza kulifungia milele akitumia Sheria ya Magazeti inayoendelea kupingwa na wadau.
Nape alitangaza uamuzi huo jana, ikiwa ni siku moja baada ya habari kusambaa kuwa Serikali imelifungia milele gazeti hilo licha ya barua iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii kutokuwa na saini ya muhusika yeyote wizarani.
Waziri Nape alisema gazeti hilo sasa limefutwa milele kutokana na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa kichochezi na kuhatarisha amani, baada ya wahariri wake kutochukua hatua za kurekebisha uandishi wao kama walivyokuwa wakionywa na Serikali kuanzia mwaka 2013.
Uamuzi huo wa kwanza kwa Wizara ya Habari tangu SAT iingie madarakani Novemba mwaka jana, ulifanywa kwa kutoa Tangazo la Serikali Namba 55 la Januari 15, 2016, ukitumia kifungu cha 25 (1) cha Sheria ya Magazeti, Sura ya 229, ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau kuwa ni kandamizi na inayominya uhuru wa vyombo vya habari.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa pale ambapo kwa maoni ya Waziri anaona kwa kuzingatia maslahi ya umma au kwa ajili ya amani au utulivu, anaweza kuagiza gazeti lisitishe uchapishaji kuanzia tarehe atakayoitaja kwenye Gazeti la Serikali.
“Sheria ya Magazeti ni mbaya kwa sababu haitoi nafasi kwa upande wa pili kujibu, huku Serikali ikiwa ndiyo mlalamikaji na hapohapo hakimu,” alisema katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alipoulizwa maoni yake kuhusu uamuzi huo wa Serikali.
“Hii ni dalili mbaya kwa Rais John Magufuli. Miezi miwili tu ameanza kufungia gazeti, miaka mitano atafungia mangapi?” alihoji Meena.
Hatua hiyo imemkera mmiliki wa gazeti hilo, Simon Mkina ambaye alisema tangazo hilo la Serikali limefanywa kwa ubabe na kuminya uhuru wa vyombo vya habari.
Sheria hiyo ni moja kati ya sheria zilizochunguzwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali, ambayo iliona kuwa Waziri amepewa madaraka makubwa bila ya kuwapo jukwaa la kupinga uamuzi wake, licha ya Katiba kumpa mwanya mtu yeyote kwenda Mahakama Kuu kuomba kuangaliwa upya kwa uamuzi huo.
Akizungumzia sababu za kulitia kitanzi gazeti hilo, Nape, ambaye ameshika uwaziri kamili kwa mara ya kwanza baada ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza, alisema uamuzi huo unatokana na mwenendo wa uandishi usioridhisha wa kuandika na kuchapisha habari zenye kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi.
Alisema Msajili wa Magazeti alifanya juhudi kuanzia Juni 2013 hadi Januari mwaka huu, kumtaka mhariri wa gazeti hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala, lakini hakubadilisha.
“Tangu mwaka 2013, Msajili wa Magazeti aliwasiliana mara nane na uongozi wa gazeti, lakini majibu waliyotoa yalikuwa yenye utata,” alisema Nape.
“Hata walipohojiwa kuhusu habari mbaya walizoandika, walijibu kuwa wana ushahidi, lakini walipoambiwa waulete hawakurudi.”
Alisema hivi karibuni waliandika habari zenye kichwa cha habari “Maalim Seif Shariff Hamad Rais Zanzibar” na nyingine iliyokuwa na kichwa kisemacho “Machafuko yaja Zanzibar”.
“Kuna habari nyingi zimeandikwa na gazeti hilo tangu mwaka 2013 ambazo zinaleta uchochezi na kuhatarisha amani na utulivu,” alisema.
Waziri huyo alisema hatua hiyo inazuia gazeti hilo kuchapishwa kwa njia nyingine yoyote, ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta, Sura ya 306.
Habari za kufungiwa kwa gazeti hilo zimekuja ikiwa ni karibu miezi miwili baada ya kampuni ya Halihalisi Publishers kuibwaga Serikali mahakamani katika kesi ya kupinga kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi. Gazeti hilo lilikuwa kifungoni kwa takriban miaka miaka mitatu.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkina alisema dunia ya sasa inayoelezwa kuwa na uhuru wa kuzungumza na kusikilizwa, inachokifanya sasa Serikali ni kurudisha tasnia ya habari ilipotoka ambako ilikuwa dhambi kusema ukweli.
Mkina alisema hali hiyo inaonyesha wazi Serikali haitaki kukosolewa, inataka kusifiwa, kitu ambacho alisema kitarudisha nyuma maendeleo badala ya kuyapeleka mbele.
“Lengo la habari ni kusukuma maendeleo, lakini kwa bahati mbaya Serikali haitaki kukosolewa. Kila kitu inataka `yes yes’ na ukisema ukweli unakuwa adui,” alisema.
“Sasa wameamua kulifungia siyo kwa muda, bali milele hadi Yesu atakaporudi.”
Naye Saed Kubenea, ambaye ni mkurugenzi wa Halihalisi Publishers iliyokuwa inasimamia usambazaji wa gazeti hilo, alisema sababu ya kufungiwa kwa Mawio ni kuandika habari za kiuchambuzi na kiuchunguzi, hasa kuhusu kinachoendelea Zanzibar.
Kubenea ambaye pia ni mbunge wa Ubungo,
alisema hii ni salamu kwa vyombo vya habari kutambua kuwa Serikali haitaki kukosolewa.
Wakati huohuo, kamanda wa polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amewataka wamiliki na wahariri wa gazeti la Mawio kujisalimisha polisi kabla hawajaongeza nguvu ya kuwasaka.
Alisema licha ya wapelelezi kuwatafuta, hadi sasa bado hawajawakamata na kuwataka wamiliki kutii agizo la kutaka kufika kituoni.
“Raia mwema ni yule ambaye anatii amri bila shuruti. Ni bora wamiliki na wahariri hawa wakafika polisi kabla hawajakamatwa,” alisema.
-
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni