Jumapili, 17 Januari 2016

ASKOFU RUWAICHI ANENA KUHUSU ZANZIBAR

Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Jude Ruwa’ichi amewataka wenye dhamana nchini, kufanya uamuzi

Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Jude Ruwa’ichi

Mtwara. Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Jude Ruwa’ichi amewataka wenye dhamana nchini, kufanya uamuzi mgumu kwa ustawi wa Tanzania, akionya kuwa iwapo Zanzibar kutawaka, Bara haitakuwa salama.

Askofu Ruwa’ichi ameyasema hayo wakati hali ya kisiasa Zanzibar ikiwa kwenye mgogoro baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Rais wa visiwa hivyo, wawakilishi na madiwani, uamuzi ambao unapingwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, huku mazungumzo ya amani yakionekana kupoteza mwelekeo.

Akizungumaa wakati wa hafla ya kusimikwa kwa Askofu Mkuu Kanisa Katoliki Mkoa wa Mtwara, Titus Mdoe mkoani hapa, Askofu Ruwa’ichi aliwataka wananchi waendelee kuombea amani, lakini wenye dhamana lazima wachukue uamuzi mgumu.

“Tuzidi kuomba amani itawale na hali inayoendelea Zanzibar tuangalie isitufikishe hatua ya kutugawa,” alisema Askofu Ruwa’ichi.

“Zanzibar pakiwaka na Bara hapatakuwa shwari. Tumwombe Mungu atuepushe na mafarakano yote yanayoweza kuharibu amani yetu.

“Wenye dhamana wafanye maamuzi magumu kwa ustawi wa jamii.”

Kukwama kwa hali ya kisiasa Zanzibar kulifanya wagombea wa urais kutoka vyama vyenye ushindani mkubwa, Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) na Dk Ali Mohamed Shein (CCM) kuanza mazungumzo pamoja na marais wa zamani wa visiwa hivyo na Jakaya Kikwete, lakini hadi sasa hakuna muafaka uliopatikana na badala yake kila upande unatoa kauli inayopingwa na mwingine.

Wakati Dk Shein anawataka Wazanzibari kuanza kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi kama yalivyoahidiwa na ZEC, Maalim Seif anataka mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 atangazwe na vyama hivyo vikutane kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Pia, Maalim Seif, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwenye serikali ya SUK inayomaliza muda wake, ameshamwandikia barua kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis kumuomba atumie ushawishi wake kutatua mgogoro huo mapema.

hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama aliyekuwa mgeni rasmi.

Lakini Mhagama hakugusia suala hilo, badala yake alisema Taifa halina maadili kuanzia ngazi ya viongozi hadi wananchi, kulitaka kanisa kuwajenga wananchi kiimani na kimaadili na kuwa Serikali itasimamia sheria na misingi ya maadili.

Alisema vitendo vya rushwa na mauaji ya albino yanapaswa kukemewa na kila mmoja.

“Tumaini la Serikali liko kwako Mdoe. Viongozi wa dini mtatusaidia kulea Watanzania kwa kufuata misingi ya dini huku sisi viongozi wa Serikali tukiwalea kwa kufuata sheria na taratibu za kisheria,” alisema.

“Tabia za kifisadi, ujambazi, kishirikina na rushwa zimeendelea kutawala nchini. Niwahakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kupambana na hayo yote,” alisema Mhagama.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni