Alhamisi, 14 Januari 2016

JOTO LAZIDI JIJINI DAR

Joto kali Dar laibua mazito

Magonjwa ya ngozi, kupungukiwa maji mwilini na maumivu ya kichwa ni kadhia zitakazowakumba baadhi

Dar es Salaam. Magonjwa ya ngozi, kupungukiwa maji mwilini na maumivu ya kichwa ni kadhia zitakazowakumba baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam kutokana na joto kali linalolikumba jiji hilo.

Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetangaza kuwa hali ya hewa katika jiji hilo hadi jana lilikuwa limefikia nyuzi joto 35.

Meneja wa Huduma za Utabiri wa TMA, Samwel Mbuya jana alisema joto la mwaka huu limevunja rekodi kwani kwa kawaida, kipindi cha Januari linatakiwa liwe nyuzi joto 32.

Mbuya alisema joto hilo pia limeongezeka hata kwa upande wa Zanzibar ambako limefikia nyuzi joto 35 ikiwa ni ongezeko la asilimia mbili.

Alisema sababu kubwa ni kuongezeka kwa joto katika ukanda wa Bahari ya Hindi ambalo pia linatishia kuwapo kwa mvua za El-nino.

Alisema kadiri mvua zinavyochelewa, ndivyo joto la bahari linavyozidi kuongezeka na kusababisha hali iliyopo.

Madhara ya joto kiafya

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani ya mwili, Meshack Shimwela alisema kwa sasa wanapokea kesi nyingi za magonjwa ya ngozi kama upele, fangasi, kupungua maji mwilini na kuumwa kichwa.

Alisema joto kali linamfanya mtu apoteze wastani wa lita tatu za maji kwa siku. “Kwa watu wasiokunywa maji katika kipindi hiki wanaweza kukaukiwa maji, kwa sababu hawanywi vimiminika vya kutosha kujazia kiwango kile kilichopotea,” alisema.     

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni