KUFURU: Messi kuanza kupokea Sh 1.7 bilioni kwa wiki
SOKA linaelekea wapi? Hakuna anayejua. Lakini sasa imefika mahala ambapo mchezaji mmoja
ADVERTISEMENT
SOKA linaelekea wapi? Hakuna anayejua. Lakini sasa imefika mahala ambapo mchezaji mmoja anakaribia kulipwa dau la Sh1.7 bilioni kwa wiki kwa mujibu wa mshahara wake.
Staa wa Barcelona, Lionel Messi ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wa kihistoria duniani anakaribia kulipwa dau la Pauni 583,000 kwa wiki ambazo ni sawa na Shilingi za Tanzania 1,778,120,000 kwa wiki na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi duniani.
Dili hilo litamfanya Messi alipwe dau la Pauni 30 milioni kwa mwaka na hivyo kumfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi kwa sasa wakati huu akiwa ameweka rekodi ya kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mara nyingi zaidi. Mara tano.
Hilo litafanyika mwishoni mwa msimu katika kipindi cha majira ya joto wakati mkataba wa mchezaji huyo utakapoongezewa vipengele upya baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ya nyongeza mwaka 2013 na mkataba huo unakoma mwaka 2018. Kwa mujibu wa kipengele kimoja cha nyaraka za mkataba wa Messi, imeandikwa kuwa mshahara wake utapandishwa mara mbili kuanzia mwanzoni mwa msimu 2016 bila ya kusaini mkataba mpya kutoka kwa huu wa sasa unaoisha 2018.
Kwa sasa Messi anaingiza dau la Pauni 17 milioni kwa mwaka lakini kwa mujibu wa mkataba huo, dau hilo linapaswa kwenda mpaka Pauni 29.8 milioni na hivyo kuzikata maini klabu mbili tajiri za Manchester City na PSG ambazo zinadaiwa kuwa katika nafasi ya kumtwaa Messi.
Dau la mshahara ambalo Manchester City walikuwa wamepanga kulitoa kwa Messi kwa sasa litakuwa pungufu kwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki lakini matumaini ya kumnasa Messi yanazidi kukatika zaidi baada ya kugundulika kuwa kama Barcelona ikiamua kumuuza staa huyo, basi suala hilo litakuja akiwa katika mshahara mpya.
ADVERTISEMENT
Kwa mujibu wa mkataba huo, Barcelona italazimika kulipa dau la Pauni 15 milioni kama fidia kwa Messi kama ikiamua kumuuza kabla ya nyongeza hiyo ya mshahara haijaanza kufanya kazi.
Licha ya dau hilo la mshahara, kwa mujibu wa Jarida la France Football la Mei 2015, Messi mwenye umri wa miaka 28 anadaiwa kukusanya kiasi cha Pauni 48 milioni kwa mwaka 2014 ukijumlisha na bonasi zake mbalimbali, mshahara na mikataba ya kibiashara.
Mauzo ya sura yake katika mikataba yake ya kibiashara kama Turkish Airlines, Fifa video Games na mingineyo yamemwongezea dau la Pauni 1.8 milioni kwa mwaka na hivyo kufikia idadi ya Pauni 21 milioni kwa mwaka.
Messi ambaye anakaribia kufikia rekodi ya staa wa zamani wa England, David Beckham ya kumaliza nafasi hiyo ya juu kwa utajiri kwa mwaka wa sita mfululizo, bado amemwacha mbali mpinzani wake wa karibu wa uwanjani, Cristano Ronaldo wa Real Madrid licha ya Ronaldo kuongeza mapato yake kwa wingi katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Ronaldo (31), aliongeza kiasi cha Pauni 11 milioni na hivyo kufikia dau la Pauni 40 milioni kwa mwaka wakati Neymar wa Barcelona ameongeza mapato yake kuanzia Pauni 21 milioni hadi 27 milioni.
Wachezaji tisa wana pato la zaidi ya Pauni 15 milioni kwa mwaka akiwemo nahodha wa PSG, Thiago Silva anayeingiza Pauni 20 milioni kwa mwaka huku staa wa timu yake, Zlatan Ibrahimovic akiingiza Pauni 15.8 milioni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni