Jumanne, 26 Januari 2016

Chenge Ndiye Mwenyekiti wa Bunge

Chenge awa mwenyekiti wa Bunge

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye aligombea uspika mwaka 2010 akisema anataka

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge,  akiwaomba wabunge wamchague kuwa mwenyekiti wa Bunge katika kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Bunge la 11, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye aligombea uspika mwaka 2010 akisema anataka kutibu majeraha yaliyoliumiza Bunge, Taifa na CCM kutokana na kashfa mbalimbali, amechaguliwa kuwa mmoja wa wenyeviti watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Chenge, ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kuingia bungeni na kuteuliwa kuwa waziri aliouachia wakati kashfa ya ununuzi wa rada ilipopambamoto, ataongoza Bunge kwa nafasi ya mwenyekiti akiwa na Dk Mary Mwanjelwa na Najma Murtaza, ambao walikuwa wagombea pekee wa nafasi hizo.

Hata hivyo, ilibidi Spika Job Ndugai amuokoe kwa kuzima swali lililohusu kashfa ya uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow lililoulizwa na mbunge kutoka Chadema, Latifa Chande.

Chenge alitajwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada baada ya taasisi ya Uingereza inayoshughulikia makosa makubwa ya jinai, kubaini kuwa alikuwa na dola 1 milioni kwenye akaunti yake iliyokuwa mjini Jersey, fedha zilizohusishwa na ununuzi wa rada hiyo ambayo bei yake ilikuzwa.

Kashfa hiyo ilimfanya Chenge alazimike kujiuzulu nafasi ya Waziri wa Miundombinu mwaka 2008, lakini Novemba, 2010 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilimsafisha na siku chache baadaye akagombea tena ubunge na kushinda.

Wakati huo aligombea uspika akisema: “Nagombea kiti cha uspika nikiamini kwamba ninao uwezo wa kutibu majeraha makubwa yaliyoumiza Bunge na Taifa, wananchi na chama changu kwa sababu tu ya kuwa kiongozi aliye tayari kujitafutia na kujitwalia umaarufu au ushujaa binafsi kwa njia ya kuwahujumu, kuwaumiza na kuwachafua wengine kwa kutengeneza tuhuma na kashfa za kila namna. Tiba ya uongozi wa aina hii ni kuchagua kiongozi bora wa Bunge.”

Hakueleza kuwa aliyekuwa akimtuhumu ni Samuel Sitta, spika wa Bunge la Tisa ambalo liliboresha kanuni na kuruhusu mijadala moto, hasa ya kashfa dhidi ya viongozi wa Serikali na kusababisha mawaziri kujiuzulu.

Mwaka juzi alijikuta kwenye kashfa ya  Tegeta Escrow baada ya kubainika kuwa aliingiziwa Sh1.6 bilioni na mmoja wa wamiliki wa IPTL na kusababisha apelekwe kwenye Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma, ambako alijaribu kulizuia lisimhoji kwa kuomba ufafanuzi Mahakama Kuu, lakini aligonga mwamba na kurejeshwa kuhojiwa.

Kashfa hiyo ilimfanya avuliwe uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, lakini alirejea tena bungeni baada ya uchaguzi wa mwaka jana.

Jana, Chenge ambaye aliwahi kujiita “nyoka wa makengeza” wakati wa kashfa ya Escrow, pamoja na wenzake wawili walikuwa wagombea pekee wa nafasi hiyo ya mwenyekiti ambayo hushikwa na watu watatu wanaomsaidia Spika kuendesha chombo hicho cha kutunga sheria.

Mara baada ya Dk Mwanjelwa kumaliza kujieleza mbele ya wabunge na kuulizwa maswali, Chenge alifuatia na alianza kubanwa swali la Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe.

“Katika Bunge lililopita CCM na wabunge walikuwajibisha kwa kashfa ya Escrow na sasa hivi unaomba kuwa mwenyekiti, siku ukiwa unaliongoza Bunge hili na hoja ya hiyo ikarudi bungeni je Utatenda haki katika kulisimamia Bunge? “ alihoji Mwabe.

Huku akicheka, Ndugai alisema hilo siyo swali jambo ambalo liliwafanya wabunge kupinga, huku wengine wakicheka. Hata hivyo alimruhusu Chenge kujibu.

“Bunge linaongozwa na kanuni na pale ambapo inakuja hoja bungeni au katika kamati zetu na inaonekana kuna masilahi fulani au inakuhusu mwenyewe, ni busara tukazingatia kanuni,” alisema Chenge.

“Ni vyema nafasi (ya mwenyekiti) ikashikwa na mwingine ili shughuli za Bunge zisiwe na makandokando yoyote. Ningeweza kusema zaidi ya hapo ila naomba niishie hapo.”

-

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni