Jumapili, 24 Januari 2016

Bonde la Mkwajuni Wagoma Kuhama Licha Ya Kubomolewa Nyumba Zao

Wakazi Bonde la Mkwajuni wagoma kuondoka

Wakazi wa Bonde la Mkwajuni katika Mtaa wa Hananasifu na Suna, Manispaa ya Kinondoni ambao nyumba

 Dar es Salaam. Wakazi wa Bonde la Mkwajuni katika Mtaa wa Hananasifu na Suna, Manispaa ya Kinondoni ambao nyumba zao zilibomolewa, wanaishi kwenye eneo hilo licha ya kuendelea kuathiriwa na mvua.

Wakazi hao ambao hivi karibuni vibanda vyao vilibomolewa kwa amri ya Serikali, wameendelea kubakia na kujenga vibanda juu ya vifusi vya nyumba zilizobomolewa.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Nicolata Myanga alisema hawataondoka eneo hilo kwa kuwa Serikali haijawapa viwanja.

“Serikali kama inataka tuondoke ije itege bomu tu hapa tufe, tutakwenda wapi? Tunaambiwa tumepewa viwanja viko wapi? Hivi kweli mimi na uzee wangu huu nimepewa kiwanja naambiwa ondoka nitang’ang’ania hapa ili iweje?” alihoji Myanga mwenye umri wa miaka 68.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Magreth Dimoso alisema hali ya maisha yao inazidi kuwa ngumu kila siku, lakini mbaya zaidi ni kuwa kadri mvua zinavyonyesha hawana pa kukimbilia kwa kuwa hata baadhi ya vibanda walivyojenga vimesombwa na maji.

Mwathirika mwingine wa bomoabomoa hiyo, Anastatus Mponda alisema maisha yao ni magumu kuliko hata ya wakimbizi.

Maisha ya ombaomba

Kutokana na hali ngumu waliyonayo, baadhi yao wamegeuka kuwa ombaomba, kwani hata mwandishi wa habari hizi alipofika alilakiwa kwa salamu ya kuombwa Sh1,000 na Jumanne Iddy.

Maimuna Juma aliyekuwa amekaa nje ya kibanda chake akiwa anambembeleza mwanaye aliyekuwa akilia kwa sababu ya njaa, alipomuona mwandishi aliomba msaada wa fedha akamnunulie chakula.

Uongozi wa mtaa wanena

Mwenyekiti wa Mtaa wa Suna, Salumu Hamis alisema kuwa kuna kaya zaidi ya 700 zinaishi sehemu hiyo na kwamba, kati ya jumla ya kaya 900 zilizokuwa zinaishi hapo, 150 pekee ndizo zilipewa viwanja Mabwepande,” alisema

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni