Jumamosi, 30 Januari 2016

Panga La JPM Laondoa Vichwa 152

Panga la JPM lachinja vichwa 152

Hakuna shaka kuwa Rais John Magufuli anatimiza ahadi yake ya kutumbua majipu aliyoitoa katika

Rais John Magufuli.

Dar es Salaam. Hakuna shaka kuwa Rais John Magufuli anatimiza ahadi yake ya kutumbua majipu aliyoitoa katika hotuba yake ya kwanza bungeni baada ya zaidi ya watumishi 152 wa Serikali kutimuliwa hata kabla ya siku 100 kutimia.

Hao ni watumishi waliotimuliwa kwa majina au vyeo vyao, lakini ukijumlisha na wengine waliosimamishwa au kufukuzwa kwa matamko bila kutajwa majina, idadi ni kubwa zaidi.

Watumishi hao wamesimamishwa na baadhi wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma, Rais kutoridhishwa na utendaji wao, wizi kwenye taasisi zao, ukwepaji kodi, tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma na utovu wa nidhamu.

Hatua hizo ni utekelezaji wa ahadi ambazo Rais Magufuli alitoa kwenye hotuba yake ya kwanza bungeni Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma, alipoahidi kupambana na rushwa bila kigugumizi wala haya yoyote.

“Dawa ya jipu ni kulitumbua na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine,” alisema.

Timuatimua hiyo, ambayo ilimgusa katibu mkuu wa wizara, wakurugenzi wa taasisi na watumishi waandamizi, ilifanywa pia na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na baadhi ya mawaziri wa JPM.

Hadi sasa, taasisi zilizopewa jukumu la kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani watumishi walioonekana na matatizo, bado hazijatoa taarifa wala kuchukua hatua.

Akizungumzia kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-Utumishi wa Umma, Florence Temba alisema iwapo Rais, Waziri Mkuu au Waziri ameagiza mtumishi asimamishwe kazi, huanza kuangaliwa wakati uchunguzi unafanyika.

Alisema iwapo kiongozi atasema mtumishi amefukuzwa kazi, ni dhahiri kuwa huyo ameondolewa kabisa katika ajira za Serikali.

“Hata hivyo, baadhi ya wanaosimamishwa huweza kuendelea kulipwa mishahara yao kulingana na mazingira ya kesi zao,” alisema.

Bosi wa Muhimbili

Hatua za kusimamisha na kutimua zilianza siku nne tu baada ya Rais kuapishwa, ambapo Novemba 9, 2015 alimsimamisha kazi kaimu mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hussein Kidanto, na kuivunja bodi hiyo iliyokuwa na wajumbe 11.

Rished Bade

Rais Magufuli alimfukuza kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade Novemba 27.

Bodi ya TPA

Desemba 7 , mwaka jana, Magufuli alivunja bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadh Massawe.

Bodi ya TPA ilikuwa na wajumbe wanane, ambao ni Dk Tulia Ackson, ambaye sasa ni Naibu Spika wa Bunge, Mussa Ally Nyamsingwa (Mhandisi wa Ujenzi), Donata Mugassa (mtaalamu wa ununuzi na mjumbe wa Bodi ya Posta), na Haruna Masebu (mkurugenzi mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Wajumbe wengine ni Flavian Kinunda, Mhandisi Gema Modu, Dk Francis Michael na Crescentius Magori.

Pia, aliwasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD) ambao ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante na James Kamwomwa.

Wengine ambao hawakuwamo kwenye ripoti hiyo ambao ni viongozi wa sekta zilizotoa ruhusa makontena kutoka ndani ya bandari lakini ni wahusika wakuu ni Shaban Mngazija aliyekuwa meneja mapato, Rajab Mdoe (mkurugenzi wa fedha na mkuu wa Bandari Kavu), Ibin Masoud (kaimu mkurugenzi wa fedha), Apolonia Mosha (meneja msaidizi wa Bandari-Fedha). Jumla ya waliotimuliwa TPA na TRA ni 47.

Dk Hoseah

Akiendelea na kasi yake ambayo ameipa jina “kutumbua majipu”, Desemba 16, 2015 Rais alitengua uteuzi nafasi nyeti ya mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah. Rais alisema alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa Takukuru chini ya mkurugenzi huyo.

Maofisa wengine wa taasisi hiyo walisimamishwa kazi kwa kukiuka maagizo yaliyohusu safari za nje. Waliosimamishwa kazi ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas, wakiwa watumishi waandamizi wa taasisi hiyo.

Bosi wa Rahco

Rais JPM alimsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za Reli Tanzania (Rahco), Benhadard Tito Desemba 23, 2015 kwa kile kilichoelezwa ni “ukiukwaji mkubwa wa taratibu za ununuzi” katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati. Pia alivunja bodi ya Rahco yenye wajumbe wanane na bodi ya TRL yenye wajumbe wanane pia.

Katibu tawala Mwanza

Akiendelea na kasi hiyo, Januari 15, alitengua uteuzi na kumfukuza kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Faisal Issa kutokana na “utovu wa mkubwa wa nidhamu” aliounyesha katika kikao cha cha kamati ya ulinzi kilichofanyika mjini Mwanza.

Idara ya Uhamiaji

Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia utawala na fedha, Piniel Mgonja Januari 21 ili kupisha uchunguzi baada ya kubaini dosari kadhaa kwenye ofisi hiyo.

Mkurugenzi Nida

Utumbuaji huo wa majipu haukushia hapo. Januari 25, Dk Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu kutokana na matumizi yasiyoridhisha ya Sh179 bilioni.

Wengine waliosimamishwa Nida ni Joseph Makani ambaye ni mkurugenzi wa Tehama, Rahel Mapande (ofisa ugavi mkuu), Sabrina Nyoni (mkurugenzi wa sheria) na George Ntalima, ofisa usafirishaji.

Pia, aliwarudisha nyumbani mabalozi wawili, Dk Batilda Buriani aliyekuwa Japan, Dk James Msekela (Roma, Italia). Pia, Peter Kallaghe (Uingereza) na kurejeshwa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano, Kikanda na Kimataifa.

Waziri Mkuu

Wakati Rais Magufuli akitimua watumishi hao wa umma, Novemba 27, mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimsimamisha kazi Kamishna wa Kodi na Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki, Habibu Mponezya wa kitengo cha huduma kwa wateja, Haruni Mpande na Hamis Ali wa kitengo cha Tehama na Eliachi Mrema wa Bandari Kavu. (ICD).

Baadaye Novemba 29, Majaliwa aliwafukuza wafanyakazi watatu wa TRA, Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.

Kigoma

Majaliwa aliwasimamisha watumishi tisa wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Januari 8 kwa tuhuma za kuingia mikataba mibovu isiyokuwa na tija na kuisababishia manispaa kupoteza mapato. Pia wanatuhumiwa kulipa fidia batili na kuuza mali za halmashauri kinyume cha sheria.

Ruvuma

Kadhalika, akiwa mkoani Ruvuma Januari 8, Majaliwa alimsimamisha kazi meneja uendeshaji wa kiwanda cha kusindika tumbaku (Sontop), Paul Balegwa akidaiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine kufanya ubadhirifu wa fedha za wakulima na hivyo kiwanda hicho kusitisha uzalishaji kwa zaidi ya miaka 18 iliyopita.

Mawaziri

George Simbachawene (Tamisemi) alimsimamisha kazi mtendaji mkuu mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Asteria Mlambo.

Waziri huyo pia alitoa agizo la kusimamishwa kwa ofisa biashara wa Manispaa ya Ilala, Dennis Mrema. Hali kadhalika, Mkurugenzi wa Manispaa za Kigoma, Mhandisi Boniface Nyambele na mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Suleiman Lukanga.

Simbachawene pia aliwasimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Augustino Kalinga na wenzake kaimu ofisa biashara wa manispaa hiyo, Elias Kamara na Donatila Vedasto kwa kosa la kusababisha urasimu katika utoaji wa leseni za biashara.

Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), amewasimamisha kazi wafanyakazi 15 wa Mamlaka ya Bandari kwa tuhuma za upotevu wa Sh48 bilioni.

Wizara pia iliwasimamisha wakuu wanne wa idara wa kampuni ya huduma za meli (Marine) kwa tuhuma ya ubadhirifu wa zaidi ya Sh600 milioni.

Profesa Jumanne Magembe (Maliasili na Utalii), amemsimamisha kazi mkurugenzi wa mipango na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu wa wakala wa misitu nchini, Mohammed Kilongo na maofisa wa misitu wa mikoa yote nchini.

Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi), amemtimua mkuu wa mnada wa mifugo wa Pugu na watumishi walioshiriki kuiba ushuru wa Serikali.

Pia aliagiza viongozi tisa wa vyama vya ushirika vya Mfyome, Magubike, Kiwemu, Kitai, Mhanga na Kampuni ya Umoja wa Wakulima wa Tumbaku Iringa (ITCOJE Ltd), wakabidhi ofisi zao kutokana na tuhuma za kutapeli trekta za mkopo.

Ummy Mwalimu (Afya), amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Diwani Msemo.

Jenista Mhagama (Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), alimtimua mkandarasi wa mfereji wa Buguruni kwa Mnyamani.

Simiyu

Januari 29, Rais John Magufuli aliwafukuza kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Bariadi, Erica Mussika kwa shindwa kusimamia mradi mkubwa wa barabara wa Sh9.192 bilioni, uliofanikishwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia na amemfukuza kazi Mhandisi wa ujenzi, Ruben Muyungi.

Maoni ya wasomi

Akizungumzia hatua hizo, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema anapata shaka na aina hiyo ya utendaji.

“Labda kwa Rais ambaye huenda akawa na mkono mrefu wa kupata taarifa kuhusu watendaji anaowachukulia hatua, ila kwa hao wengine napata shaka,” alisema.

Salim alisema anachokiona kwa mawaziri ni ushabiki wa kuiga staili ya utendaji wa Rais Magufuli, ili waonekana wanafanya kazi.

Naye, Dk Benson Bana alisema maamuzi hayo yana matokeo ambayo ni ya sura mbili, hasi na chanya.

Dk Bana, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kufanya hivyo kutasababisha watumishi wa umma wafanye kazi kwa woga.

Alisisitiza kuwa kwa wale wanaosimamishwa kupisha uchunguzi, unapomalizika na mtumishi akibainika hana hatia, basi atangazwe kuwa amerejeshwa kazini kuliko mambo kufanyika kimyakimya.

“Kwa sasa wafanyakazi wanafanya kazi wakiwa na hofu kwamba huenda waziri atatokea itakuwaje, “ alisema Bana.

Akizungumzia matokeo chanya, alisema hatua ya kuwajibishwa watendaji hao, imerejesha utendaji mzuri katika ofisi za umma kwa sababu kuna baadhi zilikuwa zimekithiri ufisadi, rushwa na uzembe.

-

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni