Jumatatu, 11 Januari 2016

ASKOFU KWANGU AENDELEA KUTAMBULIKA NA KANISA LA ANGLIKANA

Anglikana waendelea kumtambua Askofu Kwangu

Kanisa la Anglikana Tanzania limekanusha tuhuma za kumfukuza Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya

Dodoma. Kanisa la Anglikana Tanzania limekanusha tuhuma za kumfukuza Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Victoria Nyanza na kusema waliotoa tamko la kumfukuza Askofu Boniface Kwangu ni kikundi cha  watu waliokosa fadhila.

Jana katika vyombo mbalimbali vya habari kulikuwa na taarifa za kufukuzwa kwa Askofu Kwangu kwa kile kilichoelezwa ni ubadhilifu wa zaidi ya Sh500 milioni  kutoka katika miradi ya Kanisa.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa nyumba ya wahudumu wa Kanisa Mchungaji Andrew Kashilim  ambaye alisema kuwa  kumekuwa na malalamiko mengi juu ya Askofu Kwangu lakini  Uongozi wa juu umekuwa  hauyafanyii kazi.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Anglikana Mchungaji Canon Johnson Chinyong’ole jana aliitisha vyombo vya habari na kulaani kitendo hicho na kusema kimekiuka Katiba ya Anglikana Tanzania kifungu cha tisa  ibara ya (1) na ibara ndogo (a) kinachoeleza kuhusu madaraka ya Askofu Mkuu.

“Askofu Mkuu zaidi ya madaraka aliyo nayo kama Askofu wa Dayosisi, atakuwa na madaraka yafuatayo:- (a)Uongozi na uangalizi wa Kanisa zima na Maaskofu wake kwa kufuata Katiba hii, kutokana na Katiba hiyo, hakuna mchungaji yoyote anayeruhusiwa  kutoa tamko lolote pasipo kibali cha Askofu Mkuu,” ilisomeka sehemu ya tamko hilo.

Mchungaji Chinyong’ole alisema Katiba ya Anglikana jimbo na ya Dayosisi zinaelekeza njia ya kumfukuza Askofu kwamba ni kumtaka ajiuzuru au kustaafu sio kumfukuza.

“Kanisa Anglikana Tanzania linatoa onyo kwa kwa wachungaji waliofanya hivyo wasirudie tena kulipotosha Kanisa na umma wa Watanzania, waache Katiba ya Kanisa itumike kufikia maamuzi bila ya kuleta machafuko ili kujenga Kanisa la Kristo kwa utukufu wa Mungu,” alisema Chinyong’ole

Hata hivyo alikiri kuwa Kanisa linamtambua Mchungaji Kashilimu kuwa ni kiongozi wa nyumba ya huduma kwa mujibu wa Katiba lakini wakasema tatizo lake ni kujichukulia uamuzi bila ya kufuata taratibu.

Licha ya kukiri kuwa uongozi wa Dayosisi hiyo ulishapeleka malalamiko kwa muda mrefu katika ngazi ya juu na kwamba wanaendelea kushughulikia, lakini Katibu huyo alisema Alhamisi ya Januari 7, mwaka huu walikuwa na halmashauri kwenye dayosisi na jambo hilo liligusiwa.

“Mimi pamoja na Askofu Mkuu (Dk Jakob Chimeledya) tulikuwa kwenye halmashauri yao na tuliwasihi sana kuwa jambo lao linafanyiwa kazi hivyo watulie na kingine Askofu wao amebakiza miezi mitano tu kuwa nje ya nchi akirudi mambo yote yatakwisha, sasa iweje leo washindwe kuwa na subira,” alisema.

Askofu Kwangu ameshawahi kupata msukosuko mwingine kama huo wa kutakiwa aanchie ngazi jaribio lililoshindikana Septemba 2012.

Na kwa upande wa Kanisa la Anglikana kunaonekana kuwepo na migogoro ya mingi ambayo haijafanyiwa kazi bado ikiwemo sakata la waumini wa Dayosisi ya Dar es Salaam ambalo pia lipo katika uongoziwa juu na waumini wanasubiri hatma yake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni